Taarifa za Kukanganya kuhusu Hali ya Afya ya Raila
22/06/2020 23:30 in News

Wakenya wanaendelea kutoa hisia mbalimbali kuhusu taarifa zilizoibuka mitandaoni zikisema Kinara wa ODM Raila Odinga yuko katika hali mahututi.

Baadhi ya wanabloga hasa waliowahi kufanya kazi katika Ikulu akiwamo Dennis Itumbi, wamesema Raila alisafirishwa hadi Abu Dhabi kwa ndege aina ya 4YPAA- Cessna 680 kwa ajili ya matibabu ya dharura.

Aidha, inaarifiwa kwamba Raila alisafiri pamoja na binti yake mmoja na walinzi wa binafsi kupitia Uwanja wa Ndege wa Wilson, Naorobi.

Hata hivyo, katika mtandao wake Afisa wa Mawasiliano katika ODM Philip Etale amepuuza taarifa za kusema Raila anaugua.

Badala yake, Etale amesema Raila yuko Kinshasa, DRC kwa ajili ya Mkutano unaohusiana na Usimamizi wake wa Ujenzi na Miundo Msingi Barani Afrika.

Awali nakala kadhaa zilizodaiwa kutoka kwa Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna ziliarifu kwamba Odinga yuko salama baada ya kuhudumiwa alipoanza kuwa mgonjwa asubuhi ya Jumatatu.

Haya yamejiri wiki moja tu baada ya Raila kupimwa na kusemekana kwamba hana Virusi vya Korona.

COMMENTS